BAADA ya timu ya taifa ya Tanzania , Taifa Stars kutoshana nguvu na timu ya taifa ya Ethiopia katika mchezo wa kuwania kufuzu AFCON 2025 Hemed Morocco, Kaimu Kocha Mkuu wa Stars amesema kuwa wamecheza na tim ngumu hivyo haikuwa rahisi kupata matokeo mazuri.
Baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Mkapa Septemba 4 2024 umesoma Tanzania 0-0 Ethiopia hivyo hakuna aliyeibuka na ushindi kwenye mchezo huo ambao ulikuwa na ushindani mkubwa.
Katika dakika 45 za mwanzo timu zote mbili hakuna ambayo ilipiga shuti lililolenga lango huku kipindi cha pili katika dakika za lala salama wachezaji wa Tanzania walifanya majaribio yaliyokuwa na hatari ikiwa ni kupitia kwa Clement Mzize na Mudathir Yahya lakini hayakuleta matunda kwa Tanzania.
Morocco amesema: “Ulikuwa ni mchezo mgumu na tulikuwa tunatambua kwamba tunacheza na timu ngumu hivyo haikuwa rahisi kupata matokeo lakini huu ni mpira tumetengeneza nafasi hatujatumia tunaamini tutafanya vizuri kwenye mechi zijazo.”