FELIX SIMBU ASHINDWA KUTAMBA KWENYE OLIMPIKI PARIS, TAMIRAT TOLA WA ETHIOPIA ASHINDA – VIDEO

Mshindi namba tano wa mashindano ya Olimpiki ya majira ya joto mwaka 2016 jijini Rio de Janeiro, Mtanzania Alphonce Felix Simbu ameshindwa kutamba kwenye Olimpiki ya mwaka huu jijini Paris, baada ya kumaliza nafasi ya 17 kwenye mbio ndefu za wanaume akitumia muda wa saa 2:10:03.

Licha ya kumaliza nafasi ya 17 kwa muda huo, Simbu ameongeza muda wake kutoka saa 2:11.15 alipomaliza nafasi ya tano Olimpiki ya Rio de Janeiro 2016, saa 2:11:35 alipomaliza nafasi ya saba Olimpiki ya Tokyo 2020 hadi muda wa 2:10:03 Olimpiki ya Paris 2024.

Kwa upande wa Mtanzania mwingine Gabriel Geay yeye ameshindwa kumaliza mbio hizo pamoja na bingwa mtetezi wa mbio hizo Mkenya Eliud Kipchoge ambaye alishinda medali ya dhahabu kwa kumaliza wa kwanza kwenye Olimpiki mbili mfululizo ile ya Rio de Janeiro 2016 na ya Tokyo 2020.

Mshindi wa kwanza wa mbio hizo ni Tamirat Tola wa Ethiopia ambaye ametumia muda wa saa 2:06:26 akiweka rekodi mpya ya Olimpiki na kuivunja rekodi iliyokuwepo ya muda wa saa 2:06:35, nafasi ya pili imeenda kwa Bashir Abdi wa Ubelgiji aliyetumia saa 2:06:47 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Mkenya Benson Kiptruto akitumia muda wa saa 2:07.00.

Matumaini ya Tanzania kuvunja mwiko wa kutoshinda medali ya Olimpiki baada ya miaka 43 sasa yamesalia kwa wanariadha wawili wakike, Magdalena Shauri na Jackline Sakilu watakaokimbia kesho jumapili kwenye mbio ndefu za wanawake.

Mara ya mwisho kwa Tanzania kushinda medali ya Olimpiki ilikuwa Olimpiki ya mwaka 1980 jijini Moscow pale Suleiman Nyambui aliposhinda medali ya fedha kwenye mbio za mita 5000 na Filbert Bayi aliposhinda medali ya fedha kwenye mbio za mita 3000.