RAIS wa Klabu ya Yanga Eng. Hersi Said ameweka wazi kuwa anaishukuru Serikali kwa kugharamia gharama za mashabiki kuelekea Afrika Kusini kwa ajili ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns unaotarajiwa kuchezwa Aprili 5 2024.
Ikumbukwe kwamba mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Mkapa Machi 30 baada ya dakika 90 ubao ulisoma Yanga 0-0 Mamelodi Sundowns hivyo mchezo wa mkondo wa pili utaamua nani atasonga hatua ya nusu fainali na tayari kikosi cha Yanga na masfara wa mashabiki safari wameanza.
Injinia amesema: “Tunafahamu Klabu yetu ya Young Africans SC ina mchezo mwingine wa pili kule Afrika Kusini hivyo Uongozi wenu umefanya jitihada za kupeleka Ombi katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo chini ya Waziri wetu MDamas Ndumbaro la kusafirisha mashabiki kwa njia ya Basi na tunaishukuru Wizara kwa kukubali Ombi letu.
“Wizara itahudumia gharama zote za safari ya kuelekea Afrika Kusini yenye Wanachama na Mashabiki wetu 48 kuanzia nauli mpaka pesa ya kujikimu, hivyo sisi Yanga tunaishukuru sana Wizara.
“Hapo mwanzo tulitangaza watu watakaosafiri walipaswa kuwa na shilingi laki 6 na tulipata watu 30, niwahakikishie baada ya Wizara kukubali kusafirisha Wanachama na Mashabiki wetu, zile laki 6 zitarudishwa kwa wenyewe.
“Niwatakie safari njema na nina imani safari yetu ya kurudi itakuwa nzuri kwakuwa tutarudi tukiwa tayari tumeshafuzu hatua ya nusu Fainali,”.