MWAMBA ALVES AKUTANA NA HUKUMU HII

MAHAKAMA ya juu ya Catalonia nchini Hispania imemuhukumu kutumikia jela miaka minne na nusu nyota wa zamani wa timu ya Taifa ya Brazil na Klabu ya Barcelona Dani Alves .

Alves mwenye miaka 40 amehukumiwa adhabu hiyo baada ya kukutwa na hatia ya kosa la shambulio la ngono au unyanyasaji wa kingono kwa Mwanamke mmoja kwenye Club ya usiku.

 Alves ambaye amekua rumande tangu 2023 akisubiri hukumu hii, ametakiwa kumlipa fidia ya euro 150,000 (Tsh milioni 414) Mwanamke huyo.

Ipo wazi kuwa Dani Alves ni mchezaji namba mbili mwenye makombe mengi zaidi duniani sasa anakwenda kupokonywa uhuru wake kwa miaka 4.

Hatojiamulia chochote kuanzia sasa, maisha yake yatakuwa chini ya ulinzi wa mwingine. Kwa miaka minne taka yake itabaki kuwa takataka.

Taka ya wenye mamlaka ndio taka. Ukiitazama sura yake, hauoni ule ukatili wake akiwa uwanjani anapambana na mawinga bora kabisa.

Kizimba kimeondoka na ule ujasiri wake wa kuweka mwili wake popote kuzuia bao ndani ya uwanja.

Uso wake umesawajika, labda anajutia kilichopelekea yote haya? Hatujui. Labda anaamini ameonewa kwa kilichotokea? Hatufahamu.

Tunachojua, kesi inayompeleka jela ni unyanyasaji wa kijinsia. Iwe ni kweli ama la, bado huu ni muendelezo wa anguko la mwanaume nyuma ya kinyago kilekile alichokizoea.

Hadithi iliyoanza kwa mwanamke kutenda dhambi ya kula tunda akiwa kwenye bustani ya Mungu.
Na mwisho mwanaume kupewa adhabu ya kuteseka duniani.

Pole Dani Alves ameandika Kasese Aziz.