HESABU kubwa zinahitajika kwenye msako wa ushindi kwa kila timu kuwa na mpango kazi wake ndani ya uwanja kusepa na ushindi, hivyo tu basi.
Mapinduzi 2024 ilikuwa ni moto wa kuotea mbali huku hesabu zikiwa kubwa kwa kila timu kuingia na mpango kazi wake kusepa na ushindi.
Hapa tunakuletea namna hesabu zilivyokuwa na kujibu kwa wengine huku maumivu yakiwa kwa Simba waliopoteza katika hatua ya fainali:-
Wanatunguliwa kila baada ya dakika 180
Mechi sita ambazo wamecheza walikomba dakika 540 huku wakifungwa mabao matatu na kufunga jumla ya mabao sita kwenye Mapinduzi 2024.
Safu ya ulinzi ilitunguliwa mabao matatu ikiwa na wastani wa kufungwa bao moja kila baada ya dakika 180 huku safu ya ushambuliaji ikiwa na rekodi ya kufunga bao moja kila baada ya dakika 77.
Kipa Ayoub Lakred kafungwa mabao mawili katika Mapinduzi 2024 huku Ally Salim akitunguliwa bao moja kwenye mchezo dhidi ya Singida Fountain Gate uliokuwa hatua ya nusu fainali.
Ngoma kakomba zote
Fabrince Ngoma kakomba dakika zote 540 kwenye Mapinduzi 2024 baada ya kuwa ni chaguo la kwanza chini ya Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha ambaye ni fainali yake ya kwanza kuiongoza Simba wakigotea nafasi ya pili.
Dakika zao Simba
Januari Mosi, JKU 1-3 Simba, Januari 3, Simba 2-0 Singida Fountain Gate, Januari 5, Simba 0-0 APR, Januari 8, Simba 1-0 Jamhuri, hatua ya robo fainali, Januari 10, hatua ya nusu fainali Singida Fountain Gate 1-1 Simba na Januari 13 fainali Mlandege 1-0 Simba.
Mlandege akili kubwa
Mlandege ni akili kubwa kwa kuwa kwenye mechi sita ambazo walicheza mbinu yao kubwa ilikuwa ni kujilinda zaidi hawakuwa na hesabu kubwa kwenye upande wa kufunga.
Mabao ambayo walifunga kwenye mechi hizo ni matatu, kwa kila mchezo kufunga bao mojamoja huku wao ukuta wao ukiruhusu mabao mawili kufungwa.
Ilikuwa ni Mlandege 0-0 Azam FC, Mlandege 1-1 Vital’O bao la Mlandege lilifungwa na Optatus Lupekenya dakika ya 45 akiwa ndani ya 18 kwa mguu wa kushoto.
Mlandege 1-1 Chipukizi ilikuwa Januari Mosi 2024 na bao la Mlandege lilifungwa na Khori Bennet dakika ya 15 kwa mguu wa kulia akiwa ndani ya 18 dakika ya 15.
Hatua ya robo fainali Mlandege ilikuwa ni Januari 7 ubao ulisoma KVZ 0-0 Mlandege katika hatua ya mikwaju ya penalti ilikuwa ni KVZ 2-3 Mlandege hatua ya nusu fainali ilikuwa Januari 9. Katika dakika 90 ngoma ilikuwa Mlandege 0-0 APR FC. Mshindi alipatikana kwa penalti Mlandege 4-2 APR FC ilikuwa ni Januari 9 2024.
Fainali ya maajabu
Kwenye mchezo wa fainali Januari 13 2024 ilikuwa n maajabu kwa Mlandege kwa kuvunja rekodi zote zilizopita kuanzia hatua ya makundi mpaka fainali.
Ni ushindi wa kwanza wanaupata mbele ya Simba ambayo ilikuwa na safu kali ya ushambuliaji na ilikuwa imefunga jumla ya mabao saba kwenye mechi sita ilizocheza.
Ndani ya dakika 540 walikuwa na wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 180 na kulibakisha taji hilo kwa kuwa 2023 waliwatungua Singida Fountain Gate kwenye mchezo wa fainali.