KIUNGO wa kazi ndani ya Azam FC, Ayoub Lyanga ameweka wazi kuwa kulikuwa na ofa nyingi mkononi mwake kabla ya kuwachagua matajiri hao wa Dar.
Ni 2020 Lyanga aliibukia ndani ya Azam FC akitokea Coastal Union ya Tanga iliyokuwa ikinolewa na Juma Mgunda wakati huo.
Miongoni mwa timu ambazo zilikuwa zinatajwa kuwania saini ya kiungo huyo mkali wa pasi za mwisho na mapigo huru katika kikosi cha Azam FC ni pamoja na vigogo wa Kariakoo Yanga na Simba.
Lyanga amesema: “Kulikuwa na ofa nyingi ambazo zilikuwa mezani lakini niliamua kuchagua Azam FC kwa sababu mbalimbali. Kikubwa ilikuwa ni nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza na kuaminika kwenye timu husika.
“Ninafurahi kuwa hapa Azam FC kwa kuwa tunapata ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi na wachezaji. Bado tutaendelea kupambana ili kufanya vizuri zaidi kwenye mechi zetu,”.
Msimu wa 2022/23 Lyanga alitengeneza jumla ya pasi 8 za mabao akiwa ni namba moja kwa waliotoa pasi nyingi katika kikosi hicho huku akitupia mabao manne.