AUCHO YAMEMKUTA HUKO

TIMU ya taifa ya Uganda kwenye mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026 imeanza kwa kupoteza mchezo wa kwanza wa kundi G dhidi ya Guinea kwa mabao 2-1.

Kiongozi wao ni nahodha Khalid Aucho anayeikipiga ndani ya kikosi cha Yanga, Uganda iliokota bao la dakika za jioni likifungwa na Seydouba Cisse katika dakika za nyongeza za kipindi cha pili.

Bao hilo la ushindi la Guinea lilikuwa la kwanza kwa Cisse anayeitumikia Leganes ya Hispania na alifunga akitokea benchi baada ya kuingia uwanjani akitokea benchi katika dakika ya 80 akichukua nafasi ya Abdoulaye Toure.

Katika mchezo huo, Guinea walitangulia kupata bao la kwanza mapema dakika ya 10 kupitia kwa Aguibou Camara lakini Uganda walisawazisha katika dakika ya 30 kupitia kwa Bayo Fahad.

Kichapo hicho cha ugenini kutoka kwa Guinea kimeifanya Uganda iwe nafasi ya tano katika msimamo wa kundi G lenye timu sita likiongozwa na Algeria ambayo jana iliichapa Somalia kwa mabao 3-1.

Kwa Aucho, kichapo hicho kimemkuta katika siku ambayo kamati ya usimamizi na uendeshaji ya Bodi ya Ligi Kuu imempa adhabu ya kumfungia michezo mitatu na faini ya shilingi 500,000 kwa kosa la kumpiga kiwiko Ibrahim Ajibu katika mchezo baina ya Coastal Union dhidi ya Yanga, Novemba 8.

Mbali na Aucho kupewa adhabu hiyo pia mwamuzi Emmanuel Mwandembwa kwenye mchezo huo kafungiwa miezi sita kutojishughulisha na soka kutokana na kushindwa kutafsiri vema sheria 17 za mpira.