SIMBA, YANGA ZAKUTANA NA RUNGU LA TFF, ZAKAMULIWA MINOTI

KAMATI ya uendeshaji na usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania katika kikao chake cha Novemba 14 imetoa maamuzi mbalimbali kutokana na mwenendo na matukio ndani ya ligi.

Katika adhabu hizo ni pamoja na faini ya milioni tano kwa Klabu ya Yanga kwa kosa la kuingia uwanjani kwa kupitia mlango usio rasmi Novemba 5 2023 mchezo wa Kariakoo Dabi.

Wakati Yanga wakikutana na adhabu hiyo  Simba imetozwa milioni moja kwa kosa la wachezaji wake kuchelewa kutoka nje ya chumba cha kuvalia suala hilo lilifanya mchezo huo kuchelewa kuanza kwa mudawa dakika 4 na kuvuruga mpango kwa warusha matangazo Azam TV.

Kibu Dennis aliyefunga bao katika mchezo dhidi ya Yanga ametozwa faini ya laki tano kwa kosa la kushangilia mbele ya jukwaa la mashabiki wa Yanga kwa kuonesha ishara ya kuwafunga.

Mbali na Kibu, Henock Inonga katozwa faini ya laki tano kwa kosa la kushangilia bao mbele ya maofisa wa benchi la ufundi la Yanga sawa na Kocha Msaidizi wa Yanga Moussa Ndao kwa kosa la kuwatolea lugha ya matusi maofisa wa benchi la ufundi la Simba.

Taarifa imeeleza kuwa Djigui Diarra naye katozwa faini ya laki tano kwa kosa la kwenda kushangilia mbele ya benchi la ufundi la Klabu ya Simba.