YANGA WAVAMIA ALGERIA LIGI YA MABINGWA

MABOSI wa Yanga, juzi walisafiri kuelekea nchini Algeria, kwa ajili ya kuwaangalia wapinzani wao CR Belouizdad waliongozana na mchambuzi wa video, Khalil Ben Youssef.

Timu hizo zinatarajiwa kuvaana Novemba 24, mwaka huu katika mchezo wa Kundi D wa Ligi ya Mabingwa Afrika, utakaopigwa nchini Algeria.

Yanga imepania kufanya vema katika michuano hiyo ya kimataifa msimu huu, baada ya ule uliopita kucheza Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Algiers.

Mmoja wa mabosi kutoka Kamati ya Mashindano ya Yanga, ameliambia Spoti Xtra kuwa, wamesafiri kwenda Algeria kwa ajili ya kuwaangalia CR Belouizdad ambao watacheza michezo miwili ya ligi kabla ya kukutana na Yanga.

Bosi huyo alisema chini ya mchambuzi huyo wa video, wataitumia michezo hiyo kuwaangalia wapinzani wao kwa lengo la kuona ubora na udhaifu walionao Belouizdad.

Aliongeza kuwa, anaamini mchambuzi huyo ataisoma vema kiufundi na kimfumo na baadaye kukabidhi ripoti kwa Kocha Mkuu, Muargentina, Miguel Gamondi kwa ajili ya kukiandaa kikosi chake.

“Mchambuzi wetu wa video ndani ya timu, Youssef pamoja na baadhi ya viongozi tayari wamewasili nchini Algeria ili kuwasoma wapinzani wetu Belouizdad.

 

“Youssef akiwa huko ataisoma Belouizdad kiufundi zaidi kwa kimfumo na kimuundo na ripoti itarudi mapema kwa Gamondi kwa ajili ya kuipitia.

 

“Gamondi ataitumia ripoti hiyo kumuongoza katika kukiandaa kikosi chake, kabla ya kukutana na Belouizdad,” alisema bosi huyo.

 

Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, hivi karibuni alizungumzia mipango ya timu hiyo, msimu huu katika michuano ya kimataifa na kusema kuwa: “Malengo yetu ni makubwa msimu huu katika michuano ya kimataifa, msimu uliopita tulicheza Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na huu, tunataka kufika Robo au ikiwezekana tucheze fainali.”