UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa wapinzani wao Al Ahly, Waarabu wa Misri wamekuja wakati mbaya ikiwa ni maandalizi ya mwisho ya mchezo wa ufunguzi wa African Super League.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Oktoba 20 2023 ukiwa na wageni wakubwa kutoka pande zote za dunia na miongoni mwao ni pamoja na rais wa Fifa Gianni Infantino.
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba ameweka wazi kuwa hiyo kwao ni heshima na wanaamini watafanya vizuri kupata matokeo chanya.
“Itawachukua wengine si chini ya miaka 50 kutufikia tulipo na hatujaridhika, tunataka nafasi ya Al Ahly ya ubora barani Afrika kuwa namba moja na tutaichukua. Hakuna kinachoshindikana kwa Mnyama akitaka jambo lake.”
“Dhamira yetu sio tu kumfunga Al Ahly, tumeshamfunga sana, safari hii tunataka kumtoa, na wamekuja wakati mbaya, wakati ambao tunataka sifa barani Afrika. Hatutamuacha salama.”
“Mpango wa kumtoa Al Ahly unaanza na wewe Mwanasimba kuja Kwa Mkapa. Siku hiyo funga shughuli zako mapema, wa kuswali tutasali pale karibu na uwanja baada ya hapo tutaingia ndani kuenjoy, kuna burudani za kutosha,”.