YANGA YABAKISHA DAKIKA 180 KULIPA KISASI KWA SIMBA

MASTAA wa Yanga chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi wana dakika 180 ambazo ni sawa na mechi mbili kabla ya kulipa kisasi kwa watani zao wa jadi Simba.

Ikumbukwe kwamba katika mchezo wa Ngao ya Jamii fainali iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Agosti 13 Yanga ilipokwa taji hilo na Simba iliyoshinda kwa penalti 3-1 baada ya dakika 90 ubao kusoma Yanga 0-0 Simba.

Timu hiyo kwa sasa ipo kwenye maandalizi kuelekea mchezo wao wa ligi dhidi ya Azam FC ambao ni Mzizima Dabi unatarajiwa kuchezwa Oktoba 22 na Yanga watakuwa wenyeji wa mchezo huo.

Kete hiyo ikigota mwisho kete inayofuata itakuwa Yanga v Singida Fountain Gate itakuwa ni Oktoba 26, Uwanja wa Azam Complex hii itakamilisha dakika 180 na mchezo unaofuata utakuwa ni Kariakoo Dabi dhidi ya watani zao wa jadi Simba.

Kikosi cha Simba kinachonolewa na Kocha Mkuu, Roberto Oliveira kitakuwa nyumbani kuwakaribisha Yanga, Novemba 5 kete itakayopigwa Uwanja wa Mkapa.

Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amesema  kuwa mechi zote ambazo wanacheza ni muhimu kupata pointi tatu kufikia malengo yao.

“Tuna mechi ngumu na zenye ushindani bila kujali tunacheza na timu ipi kikubwa ni kutafuta matokeo. Wachezaji wetu wapo tayari na wanajituma kuona tunaendeleza kasi yetu kwenye mechi zote,” amesema Kamwe.