MAMBO NI MAGUMU KWELIKWELI

PUMZI ndefu inavutwa na kushushwa taratibu mambo yanapokuwa tofauti na vile ambavyo yalipangwa kuwa. Ngumu kuwa na furaha katika nyakati ngumu ambazo hazidumu.

Kwenye ulimwengu wa msako wa pointi tatu muhimu kuna timu ambazo mwanzo wa ligi mambo yamekuwa ni magumu kwelikweli kuambulia ushindi.

Hapa tunakuletea baadhi ya timu zinazopambania kombe namna hii:-

Coastal Union

Chini ya Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera baada ya kucheza mechi tano za ligi imekomba pointi mbili kibindoni ndani a dakika 450.

Safu yake ya ushambuliaji imeokota jumla ya mabao 7 kibindoni huku ile ya ushambuliaji ikiwa imetupia mabao mawili pekee na moja kati ya mabao hayo lilifungwa na nahodha Ibrahim Ajibu dhidi ya Mtibwa Sugar, Uwanja wa Manungu.

Mambo ni magumu kwa kuwa katika dakika zote hizo 450 hawajakutana na zali la kukomba pointi tatu zaidi ya kupoteza mechi tatu na kuambulia sare mbili pekee kwenye msimamo ni nafasi ya 16.

Mtibwa Sugar

Kete yake ya kwanza ilishuhudia ubao wa Uwanja wa Manungu ukisoma Mtibwa Sugar 2-4 Simba. Iliyeyusha pointi tatu kwenye mchezo wa kwanza na kibindoni ina pointi mbili baada ya mechi tano.

Mechi mbili mfululizo iliambulia kichapo ndani ya Oktoba ilianza nyumbani kwa kushuhudia ubao wa Uwanja wa Manungu ukisoma Mtibwa Sugar 0-1 Singida Fountain Gate ilikuwa Oktoba 5 na Oktoba 8 ubao wa Uwanja wa Sokoine ulisoma Tanzania Prisons 3-2 Mtibwa Sugar.

Namungo

Cedrick Kaze, Kocha Mkuu wa Namungo ndani ya dakika 450 ashuhudia wakikomba pointi tatu. Ni sare katika mechi tatu walikomba na kichapo ilikuwa kwenye mechi mbili.

Ushindi ni rekodi anayopambania kuisaka kwenye mechi za ligi kutokana na kushindwa kushinda ndani ya dakika 90. Safu ya ushambuliaji ni mabao mawili kibindoni na wakitunguliwa mabao manne.

Tanzania Prisons

Wajelajela chini ya Felix Minziro kwenye msako wa pointi 15 katika mechi tano mavuno yao ni point nne. Safu ya ulinzi iliokota mabao 11 kibindoni huku ile ya ushambuliaji ikitupia mabao sita.

Nafasi ya 13 kwenye msimamo ipo ikiwa imekomba pointi tatu dhidi ya Mtibwa Sugar na kuambulia sare moja na kichapo katika mechi tatu.

Geita Gold

Walianza kwa kufungua pazia la ligi kwa kukomba pointi tatu mazima ugenini. Elias Maguli anashikilia rekodi ya kuwa mfungaji wa kwanza kwenye ligi msimu wa 2023/24.

Kwenye mechi tano chini ya Hemed Morocco pointi zao ni nne, kichapo kwenye mechi tatu na sare kwenye mechi moja pekee.

Kagera Sugar

Uwanja wa Kaitaba unatumika kwa mechi za nyumbani pale Bukoba. Mecky Maxime anasuka mipango kwenye kikosi hicho.

Ina pointi tano baada ya kucheza mechi tano, ushindi ni mechi moja, sare mechi mbili na kichapo ni mechi mbili. Nafasi yao ni 11.

Dodoma Jiji

Wakulima wa zabibu walikaza walipokutana na Azam FC ilikuwa kivumbi na jasho wakaambulia pointi moja. Sare kibindoni ni mbili, ushindi mchezo mmoja na kupoteza katika mechi mbili nafasi ya 10 pointi tano.

Singida Fountain Gate

Kutoka Singida wakiwa wanatumia Uwanja wa Liti kwa mechi za nyumbani, Katika kete tano ambazo walicheza, safu yao ya ushambuliaji ilitupia mabao matatu na ile ya ulinzi iliokota mabao manne.

Haijaanza kuchanganya kutokana na ubora wa wachezaji waliopo katika kikosi hicho ikiwa ni pamoja na Meddie Kagere, Bruno Gomes, mambo ni magumu kwenye safu ya ushambuliaji katika kucheka na nyavu, tusubiri na tuone.