MZEE wa saluti, Moses Phiri mkali wa kutupia kwa kutumia guu la kulia ndani ya kikosi cha Simba kaibuka na kufunga baada ya kupitisha saa 6,240 bila kuonyesha makeke yake.
Ikumbukwe kuwa saa hizo 6,240 ambazo zinapatikana ndani ya siku 260 mwamba Phiri hakupata zali la kufunga kwenye mechi za ligi alizopata nafasi ya kucheza.
Rekodi zinaonyesha kuwa mara ya mwisho Phiri kufunga ni Desemba 3 2022 Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Katika mchezo huo alifunga mabao mawili ilikuwa dakika ya 53 na 60 mabao yote alifunga akiwa ndani ya 18 ambapo Simba walikomba pointi tatu mazima.
Maumivu aliyopata kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Kagera Sugar Desemba 21 2022 Uwanja wa Kaitaba yalimpunguzia kasi yake kwani licha ya kupona na kuanza kurejea uwanjani bado hakupata nafasi ya kutupia kwenye mechi alizocheza.
Agosti 20 akitokea benchi kwenye mchezo dhidi ya Dodoma Jiji alipachika bao lake la kwanza msimu wa 2023/24 dakika ya 55 ubao wa Uwanja wa Uhuru uliposoma Simba 2-0 Dodoma Jiji.
Ipo wazi kuwa msimu wa 2022/23 Phiri alitupia mabao 10 akiwa ni namba mbili kwa nyota waliofunga mabao mengi Simba kinara alikuwa ni Saido Ntibanzokiza ambaye alifunga mabao 17 na alitwaa tuzo ya mfungaji bora sawa na Fiston Mayele wa Yanga.