HIVI NDIVYO AZAM FC WALIVYOWATULIZA SINGIDA FOUNTAIN GATE

AZAM FC ni washindi wa tatu katika Ngao ya Jamii 2023 baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 Singida Fountain Gate katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Singida Fountain Gate walikosa utulivu katika kipindi cha kwanza eneo la ulinzi jambo lililowafanya Azam FC kuwatuliza kwa bao la mapema zaidi.

Ni Prince Dube alianza kumtungua mlinda mlango wa Singida Fountain Gate  Beno Kakolanya dakika ya kwanza ikiwa ni muda mfupi baada ya mchezo kuanza.

Wakati Singida Fountain Gate wanapambana kutafuta bao la kuweka usawa nyota Abdul Suleiman, (Sopu) aliongeza chuma cha pili dakika ya 43 ukiwa ni mzigo mzito kwa wapinzani wao.

Jitihada za Francis Kazadi, Michael Chuku kwenye kuliandama lango la Azam FC zilikwama kutokana na ukuta imara uliokuwa ukiongozwa na Daniel Amoah kwa Azam FC.

Eneo la kiungo James Akamiko aliendeleza balaa lake huku kiungo Feisal Salum majaribio yake kadhaa akiwa nje kidogo ya 18 yakiwa ni miongoni mwa yaliyompa tabu Kakolanya wa Singida Fountain Gate.

Ikumbukwe kwamba Azam FC iliondolewa katika nusu fainali ya kwanza kwa kupoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Yanga iliyotinga fainali huku Singida Fountain Gate wao waliondolewa kwa penali 4-2 dhidi ya Simba.

Ipo wazi kuwa taji la Ngao ya Jamii 2023 ni mali ya Simba walioshinda kwa penalti 3-1 dhidi ya Yanga kwenye fainali Agosti 13 baada ya dakika 90 kutokufungana.