ROBERTO Oliveira, Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa anataka rekodi mpya kwa wachezaji hao kupata matokeo mapema kwenye mechi zaoili kuongeza hali ya kujiamini.
Simba kwa sasa ipo Tanga ikiungana na timu nyingine ambazo ni Singida Fountain Gate, Yanga na Azam FC zitakazoshiriki Ngao ya Jamii.
Oliveira anakibarua cha kuiongoza Simba kwenye mchezo dhidi ya Singida Fountain Gate ambao ni wa hatua ya nusu fainali mshindi wa mchezo huo atakutana na mshindi wa mchezo kati ya Yanga dhidi ya Azam FC, Agosti 13.
Mchezo wa Simba v Singida Fountain Gate unatarajiwa kuchezwa Agosti 9 2023 Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Oliveira amesema kuwa kila mchezo unakuwa na mbinu zake na mpango mkubwa ni kupata ushindi mapema kwenye mechi zote.
“Ikiwa wachezaji watapata bao mapema kuna hali ya kujiamini inaongezeka kwa wachezaji kuendelea kutafuta ushindi zaidi kwenye mchezo na hilo ni muhimu kwenye mechi zote.
“Ambacho ninafurahi ni kuona wachezaji wakiwa tayari kwa ushindani na wanatimiza majukumu kwa wakati hili ni jambo zuri na linahitaji kuwa na mwendelezo zaidi,” amesema Oliveira.
Miongoni mwa wachezaji wa Simba ambao wapo kwenye kikosi kinachotarajiwa kuivaa Singida Fountain Gate ni Moses Phiri, Kibu Dennis, Shomari Kapombe.