LEGEND Jonas Mkude ameaagwa na mabosi zake wa Simba kwa muda wa dakika moja baada ya kujiunga na Yanga.
Mkude ni ingizo jipya ndani ya Yanga akiungana na viungo wengine ikiwa ni Aziz KI, Zawad Mauya ambao walikuwa katika kikosi cha Yanga kilichotwaa ubingwa msimu wa 2022/23.
Ikumbukwe kwamba Mkude alidumu ndani ya Simba kwa zaidi ya miaka 10 akitumika kwenye eneo la kiungo mkabaji ni miongoni mwa nyota waliokutana na Thank You kutoka Simba kisha akatambulishwa Yanga.
Kwenye utambulisho wa wachezaji uliofanyika katika kilele cha Simba Day, Uwanja wa Mkapa, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally alisema kuwa ni muhimu kwa Wanasimba kumuaga Mkude.
Mkude ambaye yupo na kikosi cha Yanga kwa sasa akitumia jezi namba 19 alipokuwa Simba alikuwa akitumia jezi namba 20 .
“Kuna mchezaji ambaye amedumu Simba kwa muda mrefu ila tumeachana naye kutokana na mkataba wake kuisha anaitwa Jonas Mkude dakika moja naomba tusimame Wanasimba na tumpigie makofi,” alisema Ally.
Mkude hakuwepo eneo la tukio kuagwa ambapo awali uongozi wa Simba uliweka wazi kuwa utawaandikia barua wamiliki wa mchezaji ilia pate ruhusu ya kuwa kwenye tamasha hilo.
Mbali na tukio hilo pia Luis Miquissone alirejeshewa jezi aliyokuwa akiitumia wakati yupo Simba namba 11 huku Peter Banda akitambulishwa na jezi namba 40.