KOCHA mkuu mpya wa PSG, Luis Enrique anafikiria kujiuzulu nafasi yake baada ya mwezi mmoja tu, katika kazi hiyo huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni machafuko ambayo yanaendelea katika klabu hiyo hususani sakata la staa wa timu hiyo, Kylian Mbappe.
Ripoti kutoka nchini Hispania zinaeleza kuwa, Enrique ambaye aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa PSG mwanzoni mwa mwezi Julai amekasilishwa na machafuko yanayoendelea ndani ya klabu hiyo hususani yakimhusu, Mfaransa Mbappe na uongozi wa juu chini ya Mkurugenzi wa michezo, Luis Campos.
PSG ambao walimwondosha Mbappe katika ziara yao ya maandalizi ya msimu mpya nchini Japan na kumpiga marufuku kufanya mazoezi na wachezaji wa akiba, wamepanga kumuuza Mbappe msimu huu wa joto badala ya kumpoteza nyota huyo bure ambapo anatajwa kuwa kwenye mpango wa kujiunga na Real Madrid.
PSG ilitumai kwamba Enrique, 53, angeweza kuiongoza klabu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa, baada ya kushinda shindano hilo akiwa na Barcelona mwaka wa 2015.
Kocha huyo aliyerithi mikoba ya Christophe Galtier, ana rekodi nzuri ya kutwaa mataji kufuatia mafanikio makubwa aliyoyapata La Liga akiwa Barcelona.
Mbappe, 24, alisaini mkataba wa miaka miwili, na uwezekano wa mwaka wa tatu, kuongeza muda wake wa kusalia PSG mnamo 2022, akiikataa Real Madrid katika mchakato huo.
Hiyo ina maana kwamba mkataba wake utamalizika rasmi msimu ujao wa joto na anaweza kuondoka kwa uhamisho wa bure, bila kutimiza kipengele hiko cha mwaka mmoja zaidi uliosalia.
PSG wanaamini Mbappe ana makubaliano ya siri na Real kwamba atahamia huko kwa bonasi ya kusaini ya pauni milioni 137 – lakini hakuna ada ya uhamisho – mnamo 2024.