SHERIA MUHIMU KUFUATWA KUEPUKA KESI

MUDA hausubiri kwa sasa ukiwa unazidi kwenda kasi tayari kwa ajili ya msimu mpya ambao upo njiani.

Tunaona maandalizi kwa timu zote yanaendelea ikiwa ni pamoja na Namungo ambao wamezindua uzi wao mpya.

Yanga wao walitangulia mapema na mazoezi wameanza wakiwa na tamasha la SportPesa Wiki ya Mwananchi, Julai 22 Uwanja wa Mkapa.

Singida Fountain Gate nao wanaendelea na maandalizi kama ilivyo kwa Simba ambao wapo Uturuki, Azam FC ni Tunisia.

Kuna wakati hata machozi hayasaidii kufuta ukweli kwa kuwa utabaki kuwa ukweli hivyo ni muhimu wale ambao bado hawajaanza maandalizi wafanye hivyo.

Kwenye suala la usajili dirisha linakaribia kufungwa kwani Agosti ipo njiani huku wengine wakiwa bado hawajatambulisha wachezaji wao.

Pia kuna timu nyingine hazijatangaza wachezaji wao wapya na wale ambao watapewa mkono wa asante muda ni sasa kukamilisha.

Kutoa taarifa mapema kunawapa nguvu wachezaji kuingia sokoni kwa uhuru na kufanya maamuzi ya kupata changamoto mpya au kuja na mpango kazi mwingine.

Kuanza maandalizi mapema na wachezaji wapya kutaongeza nguvu ya wachezaji kuwa familia kwa kuwa kila mmoja ana utamaduni wake.

Wale ambao wapo kwenye mazungumzo na wachezaji wanapaswa kuzingatia taratibu ambazo zipo ili wasije kuangukia kwenye mtego wa adhabu za kufungiwa masuala ya usajili.

Hiki ni kipengele muhimu kuangalia mikataba ya wachezaji walikokuwa na kufanya mawasiliano kwa ukaribu na timu husika.

Huwa inaanza taratibu tabia ya kutengeneza kesi kisha mchezaji akishatambulishwa hapo ndipo habari mbaya zinapokuja kutokana na kila mmoja kutafuta sehemu ya kutokea.

Sheria ipo wazi kwenye masuala ya usajili hiyo inapaswa kufuatwa na timu zinatambua kuhusu biashara za wachezaji hivyo hazizwezi kuzuia suala la kuuza mchezaji kwenda kupata changamoto mpya hivyo tu basi.

Kuna nyakati kulikuwa na mvutano kuhusu mkataba wa mchezaji Bernard Morrison kuhusu kuibukia kwake Simba akitokea Yanga ilikuwa ni masuala ya kimkataba pia.

Mwisho mchezaji alipewa uhuru wa kuamua acheze timu ipi tayari alikuwa ameshasaini Simba hivyo haya ni masuala ambayo yafanyiwe kazi.