KIUNGO SIMBA MIKONONI KWA WAPELEKA MAUMIVU YANGA

KIUNGO Victor Ackpan raia wa Nigeria aliyekutana na Thank You ndani ya Simba anatajwa kuwa kwenye hesabu za mwisho kujiunga na Ihefu wapeleka maumivu kwa Yanga.

Ikumbukwe kwamba Ihefu ni watibuaji wa rekodi ya Yanga msimu wa 2022/23 walipogotea kwenye mechi 49 bila kufungwa walipokutana na Ihefu walitibua mpango wao wa kufikia mechi ya 50.

Ni Novemba 29 ubao wa Uwanja wa Highland Estate ulisoma Ihefu 2-1 Yanga na rekodi ya kucheza bila kufungwa tangu msimu wa 2021/22 ikagotea Mbeya.

Yanga waliandika rekodi yao kwa soka la Bongo na Afrika chini ya Nasreddine Nabi ambaye alikuwa kocha mkuu.

Taarifa zinaeleza kuwa mabosi wa Ihefu walitumia muda aliokuwa hapo kwa mkopo kumtazama na kumchuja kwa ukaribu.

“Akpan alikuwa ndani ya Ihefu na kwa muda aliokuwa anacheza hapo kwa mkopo akitokea Simba alikuwa anaonekana ana kitu hivyo kama makubaliano yatafikia sehemu nzuri atapewa mkataba,” ilieleza taarifa hiyo.

Tayari Ihefu imeanza kukamilisha maboresho ya kikosi hicho ikiwa imetangaza kuendelea na Lenny Kissu, Nivere Tigere,Juma Nyosso, Rashid Juma na kipa Fikirini Bakari.