MAYELE AIBUKA ATOA KAULI HII

MSHAMBULIAJI wa Yanga Mkongomani Fiston Mayele ameibuka na kutamka kuwa tuzo tano alizozishinda msimu uliopita wa 2022/23 zimethibitisha ubora wake, huku akiwashukuru viongozi, wachezaji na mashabiki wa timu hiyo.

Mshambuliaji huyo wa Yanga yupo Dar kwa sasa baada ya kuwa DR Congo alipokwenda katika majukumu ya timu ya taifa hilo, alikuwa kwenye kikosi kilichocheza dhidi ya Gabon katika mchezo wa kuwania kufuzu Afcon.

Tuzo hizo alizoshinda mshambuliaji huyo ni Mchezaji Bora, Mfungaji Bora, Bao Bora, Kikosi Bora cha msimu na Ufungaji Bora wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Mayele amesema waliokuwa wanabeza ubora wake, umethibitishwa na tuzo hizo alizozibeba katika msimu uliopita ambao kwake ulikuwa na mafanikio makubwa.

Mayele amesema kuwa ubora wake haujatosha pekee, shukrani nyingi amezitoa kwa wachezaji wenzake waliompa ushirikiano wa kutosha uwanjani ikiwemo pasi nzuri za kufunga.

Aliongeza kuwa hajaridhirika na mafanikio mazuri aliyoyapata msimu huu, bado ana mengi ya kuyafanya katika msimu ujao kama akibakia kuendelea kuichezea timu hiyo.

“Tuzo ambazo nimeshinda katika msimu uliopita, zimethibitisha ubora wangu, na hilo lipo wazi kila mtu aliona jinsi nilivyoipambania timu yangu ya Yanga na kufanikiwa kushinda Tuzo.

“Niwashukuru viongozi, wachezaji wenzangu, mashabiki pamoja na benchi la ufundi ambalo lilihakikisha ninakuwa bora wakati wote kwa kuniandaa vema kabla ya mchezo.

“Bado sijafanikiwa na haya mafanikio ambayo nimeyapata, bado nina kibarua kigumu cha kupambana ili nipite zaidi ya mafanikio haya,” amesema Mayele.