>

SIMBA YATANGAZA MDHAMINI MPYA, MKWANJA MNONO KUVUNWA

UONGOZI wa Simba leo Jui 16 2023 umemtambulisha mdhamini mpya ambaye atasimamia masuala ya utengenezaji wa jezi za timu hiyo ambayo imeshuhudia ubingwa wa ligi ukienda kwa watani zao wa jadi Yanga.

Awali mpango kazi wa jezi za Simba ulikuwa unasimamiwa na VunjaBei ambaye alikuwa akitenda kazi hiyo baada ya kushinda tenda na alitoa ajira kwa Watanzania wengi na bado anaendelea kutoa ajira kwa vijana pamoja na Watanzania kiujumla.

Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Salim Abdallah, ameweka wazi kuwa anampongeza mdhamini mpya na kumshukuru VunjaBei kwa muda waliofanya naye kazi.

“Nampongeza Sandaland kwa kupata nafasi hii, alijaribu mara ya kwanza hakufanikiwa lakini muda huu amepata. Namshukuru pia VunjaBei kwa udhamini aliotupatia,” amesema.

Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula ameweja wazi kuwa watapata bilioni mbili kwa mwaka kutokana na mdhamini huyo.

“Mashabiki walitwambia wanataka tuwe na jezi bora, zifike kwa wakati na zipatikane kila sehemu.

“Mwanzoni tulikuwa tunapata milioni 400 kwa mwaka kutokana na jezi. Akaja VunjaBei akatupa bilioni moja kwa mwaka na huyu wa sasa anakuja kutupa bilioni mbili kwa mwaka.

“Namshukuru sana Sandaland kuwa mdhamini wa jezi kwa msimu wa 2023/24.”