KMC YAPIGA HESABU HIZI HAPA

UONGOZI wa KMC umeweka wazi kuwa mechi tatu ambazo zimebaki wanahitaji matokeo ya ushindi kufanikisha malengo ya kubaki ndani ya Ligi Kuu Bara.

Timu hiyo ina pointi 26 imecheza mechi 27 kwenye msimamo ipo nafasi ya 14 vinara ni Yanga walio nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 68.

Ofisa Habari wa KMC, Christina Mwagala amesema kuwa matokeo wanayopata yanawapa maumivu kwa kuwa wanahitaji kushinda ili kubaki kwenye ligi.

“Matokeo ambayo tunapata sio mazuri kwa upande wetu kwani hii inatokana na ugumu wa ligi na kila timu kuhitaji kufanya vizuri.

“Kwa mechi ambazo zimebaki hizo tunaamini tutapata matokeo mazuri na kila kitu kitakwenda sawa, wachezaji wana ari kubwa kutafuta ushindi na kila mmoja anatambua nafasi ambayo tupo.

“Mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi kwenye hali hii benchi la ufundi linafanya kazi kwa ajili ya kuwapa mbinu wachezaji na tunaamini itakuwa hivyo,”.

Mchezo uliopita wa KMC chini ya Kocha Mkuu, Jamhuri Kihwelo ilishuhudia ubao ukisoma Dodoma Jiji 1-0 KMC ilikuwa ni Aprili 22,2023 Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.