SPORTPESA KUDHAMINI TIMU YA WABUNGE

KAMPUNI ya michezo na burudani ya SportPesa leo Novemba 30 imetoa vifaa vya michezo vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 20 kwa timu ya Bunge ambayo inatarajia kushiriki mashindano ya mabunge ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki mkoani Arusha.

Makabidhiano hayo yamefanyika katika ukumbi wa habari ofisi za Bunge kabla ya kuanza rasmi mashindano hayo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, SportPesa na vile vile ni Mwenyekiti wa Bunge Sports Club, Tarimba Abbas alianza kwa kuwashukuru SportPesa kwa udhamini wao ili kufanikisha ushiriki wa mashindano hayo.

“Hii ni mara ya pili kwa SportPesa kutoa udhamini huo ambapo mnamo mwaka 2017 walifanya hivyo kwenye mashindano ya Bunge.

“Tunapenda kuwahahakikishia mashabiki kuwa tunatarajia ushindi wa kishindo huku tukipeperusha bendera ya Bunge la Tanzania.

“Tulikaa kikao na viongozi wa timu na wamenihakikishia kwamba watafanya vizuri ili kuhakikisha wanarudi na ushindi.

“SportPesa imedhamini kwa kutoa vifaa vya timu zote 8 ikiwemo Mpira wa miguu, mpira wa kikapu, mpira wa pete, dart, kuvuta kamba pamoja na michezo mingine ikiwemo sare za viongozi.

Kwa upande wa Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania ambaye pia ni mwakilishi wa Katibu wa Bunge, Mohammed Mwanga alianza kwa kuwashukuru SportPesa kwa kuwapatia vifaa Bunge Sports Club na kuwaomba wabunge kuvitendea kazi.

“Nawatakia Kila la kheri kwenye mashindano yatakayofanyika Karatu na Arusha, safari njema. Mcheze kwa ushikamano na kuhakikisha mnaondoka na ushindi.

Meneja Uhusiano na Mawasiliano SportPesa Sabrina Msuya aliwashukuru timu ya Bunge la Jamhuri kwa kujitoa na kuunda timu mbalimbali na kuwatakia kila la kheri kwenye mashindano hayo yatakayohusisha nchi za Afrika Mashariki.

Kwa niaba ya viongozi wa Bunge Sports Club Mama Salma Kikwete aliongeza kwa kuwashukuru SportPesa na kuomba mashirika mengine kuhamasika katika michezo na kusaidia kwenye mashindano mbalimbali. Pia aliwaomba wabunge kuhakikisha wanashinda.