NADO NI MKALI AKITOKEA BENCHI

NYOTA wa Azam FC, Idd Suleiman, ‘Nado’ ni mkali wa kucheka na nyavu kwenye mechi za ligi akitokea benchi.

Nyota huyo rekodi zinaonyesha kuwa ameanza kikosi cha kwanza mechi nne ilikuwa dhidi ya Ruvu Shooting,Dodoma Jiji,Mbeya City na KMC.

Kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union,Novemba 27,2022 ubao wa Azam Complex uliposoma Azam FC 3-2 Coastal Union alitokea benchi, akatoa pasi moja ya bao na kufunga bao la ushindi lililoipa Azam FC pointi tatu.

Wakati ubao wa Kaitaba, Desemba 16,2022 ukisoma Kagera Sugar 2-2 Azam FC alitokea benchi akatoa pasi ya bao na kufunga bao moja lililoipa pointi moja Azam FC.

Aprili 7,2023 ubao wa Uwanja wa Azam Complex ulisoma Azam FC 2-1 Mtibwa Sugar alitupia bao moja alipotoka benchi kwenye mchezo huo.

Ni mabao manne ametupia na pasi mbili ambapo ni bao moja pekee alifunga alipoanza kikosi cha kwanza huku mabao matatu akifunga akitokea benchi na pasi zake zote mbili katoa akitokea benchi.