WAKIWA wamecheza mechi 25 ambazo ni dakika 2,250 watani wa jadi Simba na Yanga kila mmoja kajijengea ufalme wake katika eneo lake maalumu.
Leo Aprili 16,Uwanja wa Mkapa utashuhudia kila timu ikipambania ufalme wake kwenye upande wa ushambuliaji pamoja na ulinzi ndani ya dakika 90.
Simba uimara wao upo kwenye safu ya ushambuliaji huku makali yao yakiwa kwenye eneo la kiungo lenye nyota mwenye pasi nyingi ambaye ni Clatous Chama anazo 14 na katupia mabao matatu.
Ni mabao 60 Simba wamefunga baada ya kucheza jumla ya mechi 25 wakiwa na wastani wa kufunga bao kila baada ya dakika 37.
Ukuta wa Simba umetunguliwa mabao 14 ikiwa na wastani wa kufungwa bao moja kila baada ya dakika 160 kwenye ligi.
Yanga ni namba moja kwenye upande wa ulinzi ikiwa na ukuta imara baada ya kuruhusu mabao 11 kwenye mechi 25 katika dakika 2,250 ina wastani wa kuokota bao moja kila baada ya dakika 204.
Pia Yanga kwenye safu ya ushambuliaji sio wanyonge wametupia mabao 50 wakiwa na wastani wa kufunga kila baada ya dakika 45.
Kinara wa utupiaji ni Fiston Mayele mwenye mabao 16 kibindoni ikiwa ni rekodi huku kwa upande wa pasi za mwisho Jesus Moloko na Aziz KI hawa wanazo pasi nnenne.