BEKI HUYU YANGA KUIKOSA DABI KWA MKAPA

BEKI wa Yanga, Mamadou Doumbia raia wa Mali hatakuwa sehemu ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba unaotarajiwa kuchezwa kesho.

Sababu kubwa za beki hilo ambalo lilichomolewa kwenye mashindano ya ndani maarufu kama Chan akiwa na timu ya taifa ya Mali ni kutangulia mbele za haki kwa baba yake mzazi.

Taarifa rasmi iliyotolewa na Yanga jana ilieleza kuwa beki huyo anatarajiwa kuondoka jana kuelekea nchini Mali kwa ajili ya msiba huo.

“Klabu ya Yanga imepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha baba mzazi wa mchezaji wetu Mamadou Doumbia kilichotokea jana, (juzi) Mali.

“Mamadou anatarajiwa kusafiri asubuhi leo, (Jana) kuelekea nchini Mali kwa ajili ya kushiriki shughuli za mazishi,” ilieleza taarifa hiyo.

Beki huyo alikuwa kwenye maandalizi ya mchezo dhidi ya Simba na alipata nafasi ya kucheza kwenye mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar Uwanja wa Azam Complex kutokana na matatizo hayo hatakuwa sehemu ya wachezaji watakaocheza Kariakoo Dabi.