ALIYEMTUNGUA BAO LA MBALI MANULA AREJEA KAZINI

IKIWA zimebaki siku 12 za watani wa jadi Simba na Yanga kukutana Uwanja wa Mkapa habari njema kwa mashabiki wa Yanga ni kwamba aliyemtungua Aishi Manula bao kali akiwa nje ya 18 amerejea tayari katika ubora wake.

Ni Mapinduzi Balama alifanya hivyo Januari 4,2020 Uwanja wa Mkapa alipofunga bao hilo kwa shuti kali na katika mchezo huo timu zote ziligawana pointi mojamoja baada ya ubao wa Uwanja wa Mkapa kusoma Simba 2-2 Yanga.

Ujio wake unaweza kuwa habari mbaya kwa mashabiki wa Simba kwa kuwa wanajua kwamba akiwa uwanjani hana jambo dongo hasa kwa sifa yake ya mashuti ya mbali.

Kiungo huyo mzawa aliumia alipokuwa mazoezini na msimu wa 2020/21 hakuweza kucheza mchezo hata mmoja kwa kuwa alikuwa anapambania afya yake na kwa sasa ameshapona.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Habari cha Yanga, Hassan Bumbuli aliliambia Championi Jumatatu kuwa ni suala la muda kwa mchezaji huyo kuonekana uwanjani.

“Hali ya Mapinduzi Balama kwa sasa ipo vizuri na tayari ameshaanza mazoezi na wachezaji wenzake hivyo kurejea kwake uwanjani ni suala la muda tu,’ alisema Bumbuli.