YANGA WANATAKA KURUDI WAKIONGOZA KUNDI

WAKATI leo Aprili 2 wakiwa na kazi ya kusaka ushindi dhidi ya TP Mazembe Uwanja wa Mazembe, uongozi wa Yanga umeweka wazi kuwa unahitaji kumaliza kundi ukiwa unaongoza kundi.

Timu hiyo kwenye kundi D inaongoza kwa sasa ikiwa na pointi 10 baada ya kucheza mechi tano ikiwa sawa na US Monastir ambayo ipo nafasi ya pili.

Zote zimecheza mechi tano na kupata ushindi kwenye mechi tatu, sare moja na kila mmoja amepoteza mchezo mmoja huku Yanga wakiwa wamefunga mabao mengi ambayo ni 8 na US Monastir ni mabao 6.

Makamu wa rais wa Yanga, Arafat Haji amesema kuwa wanatambua ushindani uliopo na faida ya kupata ushindi ugenini jambo ambalo wanalifanyia kazi kwa umakini.

“Tumeondoka Tanzania tukiwa tunaongoza kundi na sasa tunahitaji kurudi tukiwa tunaongoza kundi, tunatamua faida ya kuongoza kundi hasa kwenye mechi zitakazofuata hatua ya robo fainali hilo ni muhimu kwetu.

“Wapinzani wetu wanajua kwama tuliwafunga walipokuja nyumbani nao wanajivunia kwao hilo halitupi tabu tupo tayari na tunaamini tutarudi na ushindi,”.

Wachezaji wa Yanga ikiwa ni pamoja na Fiston Mayele, Djuma Shaban, Jesus Moloko Aprili Mosi walifanya mazoezi ya mwisho kwa ajili ya mchezo wa leo.