FISTON Mayele ni mshambuliaji ambaye sio mwepesi kukata tamaa akiwa uwanjani, akikutana na makipa wenye mbwembwe huwa anawatazama kisha akishagundua tabia yao hapo anaongeza presha kwenye namna ya uokoaji na kutoa pasi.
Amekuwa bora kwa misimu miwili mfululizo na kwenye mechi zote ambazo amecheza hajui ladha ya kuonyeshwa kadi ya njano ikiwa inamaanisha ana nidhamu kubwa awapo uwanjani.
Anawapeleka wengine darasani bure bila gharama popote kokote na hana majivuno hata akikufunga yeye bado anataka kufunga tena.
Kibindoni mabao 15 anaongoza na amebakiza bao moja kuvunja rekodi ya msimu wa 2021/22 alipotupia mabao 16, inawezekana kwani mechi bado zipo mikononi mwa Yanga na ligi haijagota mwisho.
Bao lake la 15 aliwatungua Ihefu, Uwanja wa Mkapa ubao uliposoma Yanga 1-0 Ihefu alipomtungua Bakari Fikirini.