BALEKE, SAWADOGO WAFANYA BALAA SIMBA

WAKIFANYA mazoezi pamoja na timu kwa siku mbili, Kocha msaidizi wa Simba, Juma Mgunda amevutiwa na nyota wapya waliosajiliwa na timu hiyo, katika dirisha dogo msimu huu.

Nyota hao wapya waliosajiliwa na Simba, ni mastraika Jean Baleke, Mohammed Mussa na kiungo mkabaji Ismael Sawadogo.

Mastaa hao walifanya mazoezi hayo kwa Alhamisi na Ijumaa iliyopita wakijiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara waliotarajiwa kucheza jana dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Mgunda alisema kuwa amevutiwa na ubora wa wachezaji hao kwa siku hizo mbili walizofanya mazoezi ya pamoja na timu akiamini wataongeza kitu katika kikosi chao.

Mgunda alisema kuwa benchi la ufundi limefurahia zaidi baada ya kuwaona wachezaji hao wapo tayari na fiti kwa ajili ya kuanza kutumika katika michezo ya ligi na kimataifa.

Aliongeza kuwa wachezaji hao moja kwa moja wataingia katika sehemu ya wachezaji wao watakaowatumia katika michezo ijayo.

“Wachezaji wetu watatu tuliowasajili wana utimamu wa miili, hiyo inaonyesha kuwa huko walipotoka walikuwa wakicheza katika vikosi vyao vya kwanza.

“Wachezaji wa aina hiyo ndio tulikuwa tukiwahitaji katika timu, kama unavyofahamu tuna mashindano makubwa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Hivyo hatuhitaji mchezaji wakumsubiria kwa maana ya kumpa muda wa kumuangalia, hivyo hao wote wana utayari kuipambania timu yao mpya,” alisema Mgunda.