AZAM FC inayonolewa na Kocha Mkuu, Kali Ongala imeweka rekodi yake ndani ya Kombe la Mapinduzi 2023 kuwa timu iliyookota mabao mengi nyavuni kwenye mchezo mmoja kwa timu zilizo tatu bora bara.
Ilikuwa dhidi ya Singida Big Stars kwenye mchezo wa hatua ya nusu fainali ambapo walipoteza kwa kufungwa mabao 4-1 na kuondolewa katika Kombe la Mapinduzi.
Mbali na kufungwa mabao mengi pia ni timu pekee ambayo imetinga hatua ya nusu fainali mwaka huu ambapo Simba waliokuwa wanatetea ubingwa huo wakiwa nafasi ya pili na Yanga inayoongoza ligi hizi ziligotea katika hatua ya makundi.
Kipa wao Zuber Foba anaingia kwenye rekodi ya kutunguliwa mabao manne na mchezaji mmoja ambaye ni Francy Kazad ambaye alichaguliwa kuwa mchezaji bora kwenye mchezo huo uliochezwa juzi.
Azam FC itashuhudia bingwa wa Mapinduzi 2023 ikiwa kwenye makocho kwa kuwa watabaki kuwa mashuhuda.
Ongala amesema kuwa kilichowaponza kwenye mchezo wa hatua ya nusu fainali ni makosa ya safu ya ulinzi.
“Pongezi kwa Singida Big Stars kwa namna ambavyo wamepata ushindi ninaona kwamba walistahili kutokana na kupambana muda wote kusaka matokeo.
“Makosa ya safu ya ulinzi yamewapa matokeo lakini hii ni timu na makosa yote tutafanyia kazi,”.