SINGIDA BIG STARS NI WAMOTO KWELIKWELI

NGOMA ni nzito lakini inapigika kwenye Kombe la Mapinduzi 2023 ambapo Singida Big Stars wanajambo lao kwenye kombe hilo wakiwa ni wamoto kweli.

Ni timu ya kwanza kutinga hatua ya nusu fainali ikitokea bara na jambo lao ambalo waliweka wazi tangu awali ni kutwaa taji hilo, hapa tunakuletea namna ilivyo:-

Kazad balaa tupu

Mshambuliaji wao mpya Francis Kazad ana balaa kutokana na kujenga ushikaji na nyavu huku rekodi zikionyesha kwamba anaweza kusepa na kiatu cha ufungaji bora.

Kambani katupia mabao matano  na mpira wake ni mmoja kabatini baada ya kufunga hat trick kwenye mchezo dhidi ya Azam FC ambao ulikuwa ni hatua ya nusu fainali.

Bao moja aliwatungua Yanga kwenye mchezo wa hatua ya makundi ambapo walitoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1.

Ni dakika ya 22 alifunga bao lake la kwanza huku akiwatungua Azam FC dakika ya 27,53,64 na 86 kwenye mchezo huo ulikusanya mabao matano ndani ya dakika 90.

Gomes na rekodi yake

Bruno Gomez nyota wa Singida Big Stars huyu rekodi yake ni nyota wa kwanza kufunga bao ndani ya Kombe la Mapindizi 2023 ambapo alifanya hivyo kwenye mchezo dhidi ya KMKM.

Ilikuwa dakika ya 19 kwa mguu wa kulia akiwa nje ya 18 waliposhinda mabao 2-0 na bao la pili lilipachikwa kimiani na Yusuph Kagoma dakika ya 33 kwa mguu wa kulia akiwa nje ya 18.

Dakika 270 wamekiwasha

Ndani ya dakika 270 kwenye mechi tatu ambazo wamecheza wamekiwasha kwa kusaka ushindi kwa jasho kutimiza majukumu yao.

Ni mabao 7 kibindoni wamefunga wakiwa na wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 38 wakiwa uwanjani.

Ilikuwa Kundi B ambapo ilianza kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KMKM kisha ikaambulia sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Yanga na mchezo wake wa tatu ni mabao 4-1 dhidi ya Azam FC.

Majembe mapya yemeanza kazi

Timu hiyo ambayo inashiriki Ligi Kuu Bara ikiwa nafasi ya nne na pointi 37 baada ya kucheza mechi 19 majembe yake mapya yameanza kazi katika kikosi hicho.

Nyota wao Kazad huyo kazi yake imeonekana kwa kucheka na nyavu huku ingizo lao jingine jipya ni Nickson Kibabage ambaye naye anakiwasha kwenye kombe hilo.

Saprazi ilikuwa kwenye mchezo wa nusu fainali ambapo walimtambulisha rasmi kiungo Kelvin Nashon kutoka Geita Gold ambaye yeye alianzia benchi.

Fainali

Januari 13 2023 ni fainali ya Kombe la Mapinduzi ambapo waliokuwa wanalitetea taji hilo Simba mapema walienguliwa baada ya kutunguliwa bao 1-0 na Mlandege na walimaliza kundi wakiwa na pointi tatu.

Singida Big Stars itamenyana na mshindi wa mchezo wa nusu fainali ya pili ambaye ni Mlandege huyu alipenya kwa jumla ya penalti 5-4 Namungo FC baada ya dakika 90 kutoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1.

Fainali hiyo inayosubiriwa kwa shauku kubwa itachezwa Uwanja wa Amaan.

Vigogo kuwa mashuhuda

Vigogo wote ndani ya Bongo watakuwa mashuhuda wa bingwa mpya wa 2023 baada ya timu hizo kugota mwisho kwenye mashindano hayo.

Ni Simba wao mapema kabisa walianza kufungashiwa virago kisha Yanga wakafuata na Azam FC wakakamilisha mwendo.

Ofisa Habari wa Singida Big Stars, Hussein Masanza amesema kuwa wanahitaji kupata matokeo kwenye mchezo wa fainali ili wafikie malengo yao ya kutwaa ubingwa.

“Pongezi kwa wachezaji kwa kuwa wanajituma na kutimiza majukumu yao kwa namna kazi inavyofanyika wanastahili pongezi na tukipata matokeo kwenye mchezo wa fainali tutakuwa mabingwa.

“Uzuri ni kwamba wachezaji wanajituma na benchi la ufundi linafanya kazi yake kuwanoa vijana, mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi,”.

 

Imeandikwa na Dizo Click na imetoka kwenye gazeti la Spoti Xtra Jumanne, Januari 10,2023