CHUMA HIKI HAPA KINAFUATA KUTAMBULISHWA YANGA

INAELEZWA kuwa nyota anayefuatwa kutambulishwa ndani ya kikosi cha Yanga ni beki wa kazi mzawa Dickosn Job.

Nyota huyo mkataba wake unakaribia kufika ukingoni ambapo mwisho wa msimu huu utakuwa umegota mwisho.

Habari zinaeleza kuwa tayari viongozi wa Yanga pamoja na wale ambao wanamsimamia Job wamefanya mazungumzo na kufika kwenye maelewano mazuri.

Job ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi ambaye anatajwa kuwaambia viongozi wa timu hiyo kwamba anahitaji huduma ya beki huyo.

“Maelewano yapo na wamefikia hatua nzuri mpaka sasa hivyo muda wowote kuanzia sasa anaweza kutambulishwa ikiwa mkataba wake utasainiwa,” ilieleza taarifa hiyo.

Nabi hivi karibuni aliweka wazi kuwa moja ya wachezaji ambao wanafanya vizuri ndani ya kikosi hicho ni pamoja na wale wa kwenye safu ya ulinzi.

“Kwenye ulinzi ninawapongeza wachezaji kwa kuwa wanacheza kwa ushirikiano mkubwa na hili linatufanya tuzidi kupata matokeo kwenye mechi ambazo tunacheza,”.