>

NUSU FAINALI YA KUKATA NA SHOKA LEO KOMBE LA DUNIA

UFARANSA na Morocco wanakutana kwa mara ya kwanza kwenye kwenye nusu fainali ya Kombe la Dunia itakayopigwa leo Jumatano kwenye Dimba la Al Bayt huko mjini Al Khor nchini Qatar.

Ufaransa ambao ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo wanakutana na miamba kutoka Afrika ambayo imeweka rekodi ya kufikia hatua hiyo kwa mara ya kwanza.

 Wababe hao wametinga nusu fainali baada ya kufanya vyema kwenye michezo ya robo fainali. Ufaransa wametinga nusu fainali kwa mara ya saba kwenye michuano hii baada ya kuiondosha England kwa mabao 2-1.

Kwa upande wao, Morocco imekuwa timu ya kwanza kutoka Afrika kufuzu hatua hii hiyo ni baada ya kuifunga Ureno bao 1-0 na kuishangaza dunia.

KIKOSI CHA UFARANSA

Licha ya kikosi chao kukabiliwa na majeraha, Ufaransa wameonekana kuwa na nguvu katika harakati zao za kutetea ubingwa wao.

Kylian Mbappe amefanya safu za ulinzi za wapinzani kuwa hofu, hadi sasa amefunga mabao matano hadi sasa kwenye michuano hiyo, mawili mbele ya washindani wake wa karibu wanaowania kiatu cha dhahabu.

Ufaransa wamepoteza mechi moja tu hatua ya makundi kwa bao 1-0 dhidi ya Tunisia ambapo kocha Didier Deschamps alituma timu B kwa mechi hiyo kwani Les Bleus walikuwa tayari wamefuzu.

Katika hatua ya mtoano waliwaondosha Poland kwa mabao 3-1 kabla ya kuibanjua England 2-1 na sasa wako nusu fainali.

KUHUSU MOROCCO

Miamba hii ya Afrika ilimaliza kinara kwenye kundi lao ambapo walizifunga Ubelgiji na Canada kabla ya kutoka suluhu na Croatia.

Kwenye hatua ya 16 Bora Morocco waliushtua ulimwengu kwa kulifunga taifa kubwa kisoka, Hispania chini ya Kocha wao, Luis Enrique kwa penalti 3-1 katika muda wa ziada.

Ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ureno kwenye robo fainali ndio umewapeleka nusu fainali na leo watakuwa na kazi kubwa ya kupambana na kuudhihirishia ulimwengu kuwa timu kutoka Afrika inaweza kucheza fainali mwaka huu.

VIPI MATOKEO YAO

Hawa jamaa wamekutana mara 11 kabla ya leo huku Morocco wakishinda mara moja na Ufaransa mara saba, mechi tatu zikiisha sare.

Hawajawahi kukutana katika michuano mikubwa na mara ya mwisho kukutana ilikuwa sare ya 2-2 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa mwaka 2007.

REKODI YA UFARANSA KOMBE LA DUNIA

Ufaransa ndio mabingwa watetezi, walishinda mwaka 2018 huko Urusi. Pia walishinda kwenye uwanja wao wenyewe mwaka wa 1998.

Mwaka 2006 waliibuka washindi wa pili baada ya kufungwa na Italia kwa penalti 5-3, michuano ilifanyika nchini Ujerumani. Ni nchi mbili pekee – Italia na Brazil – ambazo zina rekodi ya kushinda taji la Kombe la Dunia mara mbili mfululizo.

REKODI YA MOROCCO KOMBE LA DUNIA

Morocco imefuzu Kombe la Dunia mara sita lakini haijawahi kufuzu hatua ya 16 Bora.

HALI ZA VIKOSI

Morocco walimkosa mlinzi wake wa kati Nayef Aguerd, kutokana na jeraha alilopata katika ushindi wa mikwaju ya penalti kwenye 16 Bora dhidi ya Hispania.

Kwa upande wao Ufaransa hakuna majeruhi kuelekea mchezo huu.

DONDOO

01: Olivier Giroud wa Ufaransa amefunga mabao manne kufikia sasa kwenye Kombe la Dunia la 2022, na atakuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kufunga mabao matano ndani ya msimu mmoja kwenye michuano hiyo ikiwa leo atatikisa nyavu.

5+ Ufaransa inaweza kuwa timu ya kwanza kuwa na wachezaji wawili waliofunga mabao matano au zaidi katika Kombe la Dunia kwa msimu mmoja tangu walivyofanya hivyo Brazil mwaka 2002 (Ronaldo na Rivaldo).

06:Morocco hawajafungwa katika mechi zao sita zilizopita za Kombe la Dunia (wameshinda 3, sare 3), ikiwa ni rekodi katika historia ya Kombe la Dunia kwa timu ya Afrika.