>

MESSI KWENYE KIBARUA KIGUMU KOMBE LA DUNIA

STAA wa timu ya Taifa ya Argentina Lionel Messi endapo atafanikisha kukiongoza kikosi chake leo Desemba 13,2022 kutinga hatua ya Fainali ya Kombe la Dunia ataandika rekodi yake nyingine kwenye upande wa michuano hiyo mikubwa.

Messi ambaye ni nahodha wa Timu ya Taifa ya Argentina leo ana kazi ya kukiongoza kikosi hicho kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Dunia Qatar,2022.

Ikiwa leo atafanikisha ndoto za timu hiyo kutinga hatua ya fainali itakuwa ni mara yake ya pili kufanya hivyo jambo amalo litakuwa ni rekodi kwake.

Ni mwaka 2014 Messi alifanikiwa kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Dunia na timu hiyo ilinyooshwa bao 1-0 dhidi ya Ujerumani kwenye hatua ya fainali.

Ni dhidi ya Timu ya Taifa ya Croatia inayonolewa na Kocha Mkuu Zlatko Dalic ambaye ameweka wazi kuwa hawatamuangalia sana Messi kwenye mchezo wa leo bali watakaba bila kuogopa.

Kuhusu Messi, Dalic ambaye anainoa Croatia amesema:”Namna ya kumzuia Messi? Hatutamuangalia sana yeye, ila tunajua tutafanya nini. Kitu ambacho anakipenda zaidi ni kuwa na mpira mguuni mwake.

“Kama tukifanikiwa kukifanya kile ambacho tuliwafanyia Brazil, basi hakuna haja ya kuwaogopa wapinzani wetu,’.

Ikumbukwe kwamba hii ni michuano ya tano kwa staa  Messi ambaye alianza kushiriki michuano hiyo 2006,2010,2014,2018 na sasa ni 2022 akiwa na umri wa miaka 35.

Messi ni kati ya wachezaji bora wa muda wote katika historia ya soka amepata mafanikio makubwa akitwaa mataji ya ngazi ya klabu yote huku akiwa na timu ya Taifa ya Argentina taji lake la mwisho ni Copa America 2021.

Katika mchezo wa leo wa nusu fainali ya Kombe la Dunia unatarajiwa kuwa mgumu na Argentina ina kazi ya kusaka ushindi ili kupenya mbele ya Croatia iliyogotea nafasi ya pili 2018.

Leo ni kete nyingine kwa Messi kufanikisha ndoto hizo ambapo dunia inamtazama na mashabiki wa mpira wanafuatilia kwa ukaribu mchezo huu.

Tags