>

DODOMA JIJI WATAMBA KUWATIBULIA YANGA

UONGOZI wa Dodoma Jiji umetamba kuifunga Yanga kwenye mchezo wa ligi na kuvunja rekodi ya timu hiyo kutofungwa ndani ya ligi.

Yanga chini ya Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi imekuwa na mwendo mzuri na mechi zake za ligi haijapoteza tangu msimu wa 2021/22 ilipofungwa bao 1-0 dhidi ya Azam FC.

Ofisa Habari wa Dodoma Jiji, Moses Mpunga amesema kuwa wamefanya maandalizi mazuri na wanachohitaji kwenye mchezo wao dhidi ya Yanga ni pointi tatu.

 “Tunamshukuru Mungu amejibu maombi yetu kwa kuwa tulikuwa tunataka kucheza na Yanga ikiwa haijafungwa na timu yoyote na sasa tunakutana nayo ikiwa bado haijafungwa na sisi tunataka kuvunja hiyo unbeaten.

“Tumejiandaa vizuri na tuna morali ya hali ya juu tumekuwa na mwendelezo mzuri licha ya kupoteza dhidi ya Azam FC na tulishinda mchezo dhidi ya KMC na sasa ni zamu ya Yanga.

“Mpango mkubwa ni kupata alama tatu na ule wa mwisho kabisa ni kupata alama moja ambapo hiyo itakuwa ni ushindi kwa wapinzani wetu Yanga.

“Kwa kikosi kilivyo na mipango ilivyo tutawakosa baadhi ya wachezaji ambao ni Jimmy Shoji, Aboubakhar Ngalema na Augustino Nsata hawa bado wanaendelea na matibabu,” amesema Mpunga.