>

AIR MANULA ANATUNGULIWA TU MABAO YA MBALI

KIPA namba moja wa Simba, Aishi Manula hana bahati anapokutana na Yanga kwenye mechi za ligi kutokana na kutunguliwa mabao magumu na wapinzani hao wakiwa nje ya 18.

Manula msimu wa 2022/23 amekaa langoni kwenye mechi 6 akiyeyusha dakika 540 akiwa hajafungwa kwenye mechi nne na ni mechi mbili kufungwa ilikuwa dhidi ya KMC alipofungwa mabao mawili na dhidi ya Yanga alifungwa bao moja.

Bao la kwanza kufungwa na mfungaji akiwa nje ya 18 msimu wa 2022/23 ilikuwa dhidi ya Yanga na mtupiaji alikuwa ni Aziz KI aliyefunga kwa faulo dakika ya 45 kwa mguu wa kushoto akiwa nje ya 18.

Mabao mawili ambayo alifungwa na KMC kupitia kwa Mateo Anthon na George Makang’a  wote walikuwa ndani ya 18.

Bao lingine ambalo aliwahi kufungwa na Yanga ilikuwa Machi 8,2020, Uwanja wa Mkapa, Bernard Morrison alimtungua Manula kwa pigo la faulo dakika ya 44.

Pia Mapinduzi Balama kwenye mchezo dhidi ya Simba wakati ubao wa Uwanja wa Mkapa ukisoma Simba 2-2 Yanga alimtungua Manula kwa pigo kali akiwa nje ya 18.

Ilikuwa ni Januari 4,2022 Uwanja wa Mkapa ambapo Manula hakuwa na chaguo kuokoa mchomo wa Balama wakati wakigawana pointi mojamoja.