MANCHESTER UNITED, CHELSEA ZAMUWANIA LEAO

NI Manchester United pamoja na Chelsea zimeingia katika mpango wa kuwania saini ya winga wa AC Milan na timu ya Taifa ya Ureno Rafael Leao.

Leao alikuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Italia Serie A msimu uliopita, amebakisha miezi 18 katika mkataba wake alionao kwa sasa na mabingwa watetezi wa Ligi hiyo AC Milan.

Taarifa kutoka katika viunga vya Milan zinabainisha kuwa Leao amegoma kuongeza mkataba mpya wa miaka mitano aliopewa na uongozi wa AC Milan akiwa kwenye mpango wa kusepa.

Kwa muda mrefu Klabu ya Chelsea imekuwa ikihusishwa na dili la kumsajili Leao ambapo taarifa zinadai kuwa Chelsea iliulizia huduma ya winga huyo katika majira ya kiangazi ya usajili lakini AC Milan ikatia ngumu kuwa mchezaji huyo hauzwi.

Chelsea pamoja na Man United zote zinatarajiwa kurejea na ofa mpya majira ya dirisha kubwa la uhamisho la kiangazi ili kuweza kupata saini ya winga huyo mwenye kasi na ubunifu mkubwa.