KATIKA kuhakikisha anapata matokeo mazuri ugenini dhidi ya Al Hilal, Kocha Mkuu wa Yanga, Mtunisia, Nasreddine Nabi, amepanga kufanya mabadiliko ya baadhi ya wachezaji kwenye kikosi cha kwanza kitakachocheza mchezo huo.
Timu hizo zinatarajiwa kuvaana leo Jumapili kwenye Uwanja wa Al Hilal uliopo katika Mji wa Omdurman huko nchini Sudan katika mchezo wa marudiano.
Katika mchezo huo, Yanga itaingia uwanjani kwa lengo moja pekee la kupata ushindi au sare ya kuanzia mabao 2-2 ili wafuzu makundi, baada ya kuruhusu sare ya 1-1 nyumbani.
Nabi amesema kuwa atafanya mabadiliko hayo kutokana na makosa na upungufu aliouona katika mchezo wa kwanza waliocheza wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar na kutoka sare ya bao 1-1.
Nabi amesema kuwa wachezaji hao wapya atakaowaingiza ni kutokana na mahitaji ya ufundi na kimbinu dhidi ya wapinzani wao ili kuhakikisha wanafanikisha malengo ya kupata ushindi na kufuzu makundi.
Aliongeza kuwa ana matumaini makubwa ya kupata ushindi katika mchezo huo, licha ya kuwepo ugenini kutokana na kuwepo wachezaji wengi wenye uzoefu wa michuano hiyo ya kimataifa hasa katika michezo ya ugenini.
“Nilisema kabla tunakwenda kukutana na timu bora ambayo ni Al Hilal, ni timu yenye uzoefu mkubwa wa kucheza michuano hii, pia inaundwa na wachezaji bora na benchi bora la ufundi.
“Licha ya ubora huo, lakini tulicheza kwa ubora, bahati mbaya hatukutumia nafasi zetu ambazo tulizipata zilizokuwa za wazi kwetu kufunga mabao.
“Hivyo katika kuelekea mchezo huo, nimefanya uboreshaji wa kikosi changu mazoezini sambamba na kufanya mabadiliko ya baadhi ya wachezaji katika kikosi changu cha kwanza,” amesema Nabi.