SIMBA YACHEKELEA USHINDI

SELEMAN Matola, Kocha Msaidizi wa Simba amesema kuwa ushindi ambao wameupata mbele ya Asante Kotoko walistahili na kama wagekuwa makini zaidi wangeshinda kwa mabao mengi.

Timu hiyo inayonolewa na Kocha Mkuu, Zoran Maki imealikwa kwenye mashindano maalumu nchini Sudan ambayo yameandaliwa na Klabu ya Al Hilal.

Mchezo wao wa kwanza Simba ilishinda mabao 4-2 huku kwa Simba watupiaji wakiwa ni Agustin Okra, Pape Sakho na Clatous Chama ambaye alitupia mabao mawili kwenye mchezo huo.

 Matola amesema:”Kipindi cha kwanza tulifanya makosa dakika 5 za mwanzo lakini tuliweza kurekebisha makosa hayo na kushinda mchezo wetu ambao ulikuwa na ushindani mkubwa.

“Kipindi cha kwanza baada ya kufanikiwa kurejea mchezoni tungeongeza umakini tungeshinda mabao mengi zaidi ya yale ambayo tumeyapata ila tunawapongeza wachezaji kwa kile ambacho wamekifanya.

“Mwalimu kuna kitu amekiona kutokana na mechi ambayo tumecheza na tumetumia wachezaji ambao walikuwa hawajacheza kwa muda kupata kwao nafasi kunaongeza nguvu kwenye kikosi chetu hasa kwenye mechi zijazo za kimataifa,” amesema.

Mchezo ujao wa Simba itakuwa ni Agosti 31 dhidi ya Al Hilal ya Sudan ambao ni wenyeji