Wan-Bissaka Ajiunga na Aston Villa kwa Msimu Mmoja kwa Mkopo

Aston Villa imethibitisha kumsajili beki wa kulia wa West Ham United, Aaron Wan-Bissaka, kwa mkopo wa msimu wa 2026/27, huku mkataba huo ukiwa na kipengele kinachoweza kufanya uhamisho wake kuwa wa kudumu.

West Ham United pia imethibitisha kuondoka kwa beki huyo mwenye umri wa miaka 28, ambaye sasa anarejea katika Premier League baada ya klabu hiyo kushuka daraja msimu uliopita.

Wan-Bissaka alijiunga na West Ham akitokea Manchester United mwaka 2024 na amecheza jumla ya mechi 65 akiwa na klabu hiyo.

Kufika kwake Aston Villa kunaongeza ushindani katika nafasi ya beki wa kulia, ambapo atakuwa akichuana na Matty Cash kwa nafasi ya kikosi cha kwanza.

Kocha wa Aston Villa, Unai Emery, anatarajiwa kunufaika na uzoefu wa Wan-Bissaka katika Premier League pamoja na uwezo wake wa kukaba wachezaji mmoja kwa mmoja.

Katika msimu uliopita, Wan-Bissaka alicheza mechi 25 za Premier League akiwa na West Ham, akifanya interceptions 40 na kushinda tackles 23 kati ya 33 alizojaribu.

Pia alikuwa sehemu ya kikosi cha DR Congo katika Kombe la Dunia la 2026, akicheza mechi zote nne za timu hiyo katika mashindano hayo.

Usajili huo ni sehemu ya maboresho yanayoendelea kufanywa na Aston Villa katika kikosi chake kuelekea msimu mpya wa Premier League na mashindano ya Ulaya.

Wan-Bissaka sasa anatarajiwa kuanza maisha yake mapya Villa huku timu hiyo ikijiandaa na kampeni yake mpya ya Premier League dhidi ya Brighton.