Mlinzi wa kushoto wa Simba SC, Nickson Kibabage, ameibua mjadala baada ya kuonesha tattoo ya mnyama simba mgongoni mwake, hatua inayokuja siku chache tangu kauli za mafumbo kutoka kwa Afisa Habari wa Yanga SC, Ali Kamwe.
Kamwe, akizungumza na waandishi wa habari, alidokeza kuhusu mchezaji wa zamani wa Yanga ambaye tangu aondoke klabuni hapo ameanza kuonesha kiwango kikubwa zaidi uwanjani.
“Sisi kwenye usajili tunafanya scouting nzuri, tukigundua wewe kidogo legelege tunakuacha. Kuna bwana mdogo mmoja alivyokuwa kwetu krosi hapigi, alivyoondoka anajitutumua yani! Tattoo kibao, mshamfahamu! Utagundua huyu kafika alipokuwa anapataka,” alinukuliwa Kamwe.
Kauli hiyo imechukuliwa na wengi kumlenga moja kwa moja Kibabage, ambaye kwa sasa anaonekana kuwa katika kiwango kizuri akiwa na Simba, huku akionesha kujiamini zaidi ndani na nje ya uwanja.
Hatua ya beki huyo kuonesha tattoo ya simba imezidi kuwasha moto wa ushindani kati ya Simba SC na Yanga SC, huku mashabiki wa pande zote wakitafsiri tukio hilo kwa namna tofauti.