Refa Aliyeinyima Yanga Penati Afungiwa Mizunguko Mitatu

Mwamuzi Ally Mnyupe kutoka Morogoro amefungiwa kuchezesha mechi kwa mizunguko mitatu (3) baada ya kushindwa kutafsiri ipasavyo sheria za mpira wa miguu katika mchezo kati ya Azam FC na Yanga.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kumalizika kwa sare tasa, mwamuzi huyo alishindwa kutoa penalti kwa Yanga licha ya tukio la rafu iliyofanywa na beki wa Azam, Fuentes Mendoza, dhidi ya mshambuliaji Prince Dube ndani ya eneo la hatari.

Kwa mujibu wa Bodi ya Ligi, kupitia Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, mwamuzi huyo alifanya kosa la kiufundi kwa kushindwa kutafsiri sheria za mchezo ipasavyo.

Mbali na adhabu hiyo, Yanga imetozwa faini ya shilingi milioni tano kutokana na mashabiki wake kuwarushia chupa za maji waamuzi walipokuwa wakitoka uwanjani baada ya kumalizika kwa mchezo huo.

Aidha, Azam FC nayo imetozwa faini ya shilingi milioni tano kwa kukiuka kanuni za ligi baada ya kukataa kutumia chumba rasmi cha kuvalia na badala yake kutumia njia ya kuingilia vyumbani (corridor) kabla ya kuanza kwa mchezo.