Refa Aliyeinyima Singida Penati Dhidi ya Simba Afungiwa Mizunguko Mitatu

Mwamuzi Katanga Hussein kutoka Tabora amefungiwa kuchezesha mechi kwa mizunguko mitatu (3) baada ya kubainika kushindwa kutafsiri ipasavyo sheria za mpira wa miguu.

Adhabu hiyo inatokana na tukio la mchezo kati ya Singida Black Stars na Simba SC uliochezwa katika dimba la Uwanja wa Airtel Mtipa.

Katika mchezo huo uliomalizika kwa Simba SC kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, mwamuzi huyo alishindwa kutoa penalti kwa Singida Black Stars licha ya tukio la wazi ambapo golikipa wa Simba, Djibrilla Kassali, alimfanyia madhambi mshambuliaji Joseph Guede ndani ya eneo la hatari.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi, uamuzi huo umetolewa na Tanzania Premier League Board (TPLB), kupitia Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, baada ya tathmini kuonesha kuwa mwamuzi alifanya makosa ya kiufundi yaliyokiuka sheria za mchezo.

Mbali na adhabu hiyo, Singida Black Stars pia imetozwa faini ya shilingi milioni tano kutokana na meneja wao, Othmen Najjar, kushindwa kuzingatia kanuni za mavazi kwa maofisa wa timu wakati wa mchezo huo.

Hatua hiyo inaonyesha msisitizo wa Tanzania Premier League Board katika kuhakikisha sheria na taratibu za ligi zinazingatiwa kikamilifu na wadau wote wa mchezo.