Iran Yatangaza Huenda Isishiriki Kombe la Dunia 2026

Waziri wa Michezo na Vijana wa Iran, Ahmad Donyamali, amesema timu ya taifa ya wanaume ya nchi hiyo huenda isishiriki katika michuano ya FIFA World Cup 2026 kutokana na hali ya usalama na mvutano wa kisiasa unaoendelea.

Akizungumza katika mahojiano na kituo cha televisheni cha michezo cha Islamic Republic of Iran Broadcasting (IRIB) siku ya Jumanne, Donyamali alisema mazingira ya sasa hayaruhusu Iran kushiriki katika mashindano hayo makubwa ya soka duniani.

“Kwa kuzingatia kwamba serikali hii imehusika katika kumuua kiongozi wetu, hatuna kabisa mazingira sahihi ya kushiriki Kombe la Dunia. Wachezaji wetu hawako salama, na hali iliyopo hairuhusu ushiriki,” alisema.

Aliongeza kuwa katika miezi nane hadi tisa iliyopita, Iran imekumbwa na vita viwili ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu ya raia wake, hali ambayo imeathiri kwa kiasi kikubwa shughuli nyingi za taifa hilo ikiwemo michezo.

Wakati huo huo, Rais wa Shirikisho la Soka la Iran, Mehdi Taj, naye alihoji uwezekano wa timu ya taifa kushiriki michuano hiyo, akitaja changamoto zinazowakabili wachezaji hasa upande wa wanawake.

Taj alitoa kauli hiyo baada ya wachezaji sita wa timu ya taifa ya wanawake ya Iran kupewa visa za kibinadamu na Australia kufuatia kushiriki michezo nchini humo. Alisema iwapo hali ya sasa itaendelea kuwa hivyo, itakuwa vigumu kwa Iran kutuma timu yake katika mashindano yatakayofanyika Marekani.

Kauli hizo zimeibua mjadala mkubwa kuhusu mustakabali wa ushiriki wa Iran katika FIFA World Cup 2026, wakati mvutano wa kisiasa na kiusalama ukiendelea katika eneo la Mashariki ya Kati.