Mchezaji wa klabu ya Al Nassr na timu ya Taifa ya Senegal, Sadio Mané, ametwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashindano ya AFCON 2025 baada ya kuiongoza Senegal kutwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa ushindi wa bao 1–0 dhidi ya wenyeji Morocco.
Mané ameibuka mshindi wa tuzo hiyo kutokana na kiwango chake bora katika mashindano, ambapo alifunga mabao mawili na kutoa pasi tatu za mabao (assist), mchango mkubwa uliosaidia Senegal kutwaa taji la AFCON 2025.
Ushindi huo umeifanya Senegal kutwaa ubingwa wa AFCON kwa mara ya pili katika historia yao, baada ya mechi hiyo kulazimika kuamuliwa katika dakika 30 za nyongeza, kufuatia dakika 90 za kawaida kumalizika kwa sare tasa (0–0).
Bao pekee la ushindi lilifungwa katika dakika ya 94 ya muda wa nyongeza na Gueye, aliyewavunja mioyo maelfu ya mashabiki wa Morocco waliokuwa wamejazana uwanjani.
Kwa upande wa tuzo ya Golikipa Bora wa Mashindano, mlinda mlango wa timu ya Taifa ya Morocco, Yassine Bounou (Bono), ametunukiwa tuzo hiyo baada ya kuonyesha kiwango cha juu. Bono alicheza jumla ya mechi saba na kufanikiwa kupata clean sheets tano, akiwa nguzo muhimu kwa Morocco kufika fainali.
Tuzo ya Mfungaji Bora wa Mashindano imenyakuliwa na kiungo mshambuliaji wa Real Madrid na timu ya Taifa ya Morocco, Brahim Díaz, aliyefunga mabao matano. Díaz amewapiku Victor Osimhen na Mohamed Salah, ambao walimaliza na mabao manne kila mmoja.