Asia Mustapha Afariki Baada ya Kuishi Miaka 20 Bila Figo

Habari mbaya zilizotufikia asubuhi hii ya Desemba 24, 2025 zinaeleza kuwa, mwanadada Asia Mustapha aliyesumbuliwa na figo kwa zaidi ya miaka 20 amefariki dunia.

Taarifa zilizothibitishwa na ndugu zake zinaeleza kuwa, Asia amekutwa na umauti usiku wa kuamkia leo alipokuwa amelazwa wodi ya wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Asia alipitia mateso mazito tangu alipoanza kusumbuliwa na figo mwaka 2004 ambapo figo zake zilifeli zote hivyo ikabidi mwaka 2005 apandikizwe figo moja nchini India.

Baada ya kupandikizwa figo hiyo alikaa nayo hadi mwaka 2011 ambapo ilifeli tena na kuanzia hapo amekuwa akisafishwa damu kwa kutumia mashine (dialysis).

Kutokana na changamoto alizopitia katika maisha yake kuhusiana na figo, aliamua kuandika kitabu kinachoelezea maisha yake alichokipa jina la ‘NIMEISHI BILA FIGO MIAKA 20′.

Asia alisema kitabu hicho alikiandika kwa madhumuni ya kuwapa moyo wagonjwa wa figo na kuwaeleza kuwa kuumwa siyo mwisho wa maisha, kuwaelimisha wanaowauguza wagonjwa wa figo kuhusu chakula anachotakiwa kula mgonjwa, changamoto alizopitia na mengine mengi.

Kwa taarifa zaidi kuhusu msiba huo endelea kufuatilia GLOBAL TV…