Mchezaji wa klabu ya Manchester United na timu ya taifa ya Cameroon, Bryan Mbeumo, ameripotiwa kukataa kupewa jukumu la kuwa nahodha wa timu ya taifa kuelekea michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Kwa mujibu wa taarifa kutoka karibu na kikosi hicho, Mbeumo amesema uamuzi wake umetokana na nia ya kujikita zaidi katika kiwango chake cha uchezaji uwanjani, badala ya kubeba majukumu ya ziada yanayokuja na unahodha.
Mchezaji huyo ameeleza kuwa anaheshimu sana jukumu la nahodha, lakini kwa wakati huu anaamini mchango wake mkubwa kwa timu ni kuonesha kiwango bora ndani ya uwanja, kusaidia timu kufunga mabao na kushinda mechi, bila presha ya majukumu ya kiuongozi.
“Nataka nijikite zaidi kwenye mchezo wangu na kutoa asilimia 100 nikiwa uwanjani,” imenukuliwa kauli yake.
Uamuzi wa Mbeumo umekuja wakati Cameroon ikiendelea na maandalizi makali kuelekea AFCON, michuano ambayo mara zote imekuwa na ushindani mkubwa barani Afrika. Hatua hiyo imezua mjadala miongoni mwa mashabiki na wadau wa soka, baadhi wakiona ni uamuzi wa busara, huku wengine wakiamini angeweza kubeba jukumu hilo.
Hata hivyo, viongozi wa benchi la ufundi la Cameroon wameelezwa kuheshimu msimamo wa mchezaji huyo, wakisisitiza kuwa kilicho muhimu ni mchango wake ndani ya uwanja, iwe kama nahodha au mchezaji wa kawaida.
Bryan Mbeumo ni mmoja wa wachezaji muhimu wa kikosi cha Cameroon, akitegemewa sana katika safu ya ushambuliaji kutokana na kasi, nguvu na uwezo wake wa kufunga na kutengeneza mabao.
Cameroon itaingia AFCON ikiwa na malengo ya kufanya vizuri na kurejesha heshima yake kama moja ya mataifa makubwa ya soka barani Afrika.