BASATA Yasitisha Hafla ya TMA 2025 Bila Kutoa Sababu

Leo Disemba 13, 2025 hafla ya utoaji Tuzo za Muziki Tanzania(TMA) 2025 kwa wasanii wa muziki waliofanya vizuri katika maeneo mbalimbali nchini ilitarajiwa kufanyika.

Taarifa iliyotolewa na Baraza la Sanaa Tanzania(BASATA) imeeleza kuwa zoezi hilo halitafanyika mpaka wakati mwingine.

“Tunawataarifu kuwa hafla ya TMA iliyokuwa imepangwa kufanyika tarehe 13/12/2025 imeahirishwa mpaka pale tarehe nyingine itakapotangazwa.”

Zoezi la utoaji tuzo za TMA kwa mwaka 2024 lilifanyika Oktoba 19, 2024 jijini Dar es Salaam ambapo washindi mbalimbali walitangazwa na baadae July 29, 2025 kukabidhiwa tuzo zao.

Oktoba 24, 2025 aliyekuwa Katibu Mtendaji wa BASATA Dkt. Kedmon Mapana alitangaza kuwa zoezi la tuzo litafanyika Disemba 13, 2025.

“tuzo za muziki Tanzania zitafanyika tarehe 13, Disemba mwaka 2025. Kwa hiyo baada ya uchaguzi kuisha tutakuwa na hili jambo kubwa kwenye hizi tuzo” alisema Dkt. Mapana

Pamoja na hayo sababu za kuahirishwa kwa tuzo hizi hazijatajwa na hata tarehe ya kufanyika tena imeelezwa kuwa itatangazwa.