Jumla ya Sh91 milioni mpaka sasa zimetumika kuwalipa Wachezaji mbalimbali wa timu za mpira wa kikapu zinazoshiriki klabu bingwa ya Tanzania (NBL) kupitia mpango wa Locker Room Bonus (LRB) kupitia chapa ya michezo ya kubashiri ya betPawa.
NBL kwa sasa ipo katika hatua ya nusu fainali ambapo timu nne za wanawake na wanaume zinachuana kusaka tiketi ya fainali iliyopangwa kufanyika Jumamosi kwenye uwanja wa Chinangali, Dodoma.
Timu hizo ni pamoja na mabingwa watetezi kwa upande wa wanaume, Dar City, Dodoma Spurs, Kisasa Heroes na UDSM Outsiders ambapo kwa wanawake ni Fox Divas, Vijana Queens, Don Bosco Lioness na Orkeeswa.
Timu hizo zote zimejihakikishia kucheza ligi ya taifa ya mpira wa kikapu ya mwaka 2026.
Mratibu wa Masoko wa chapa ya betPawa wa Afrika Mashariki Nassoro Mungaya amesema kuwa fedha hizo zimelipwa kwaa wachezaji ambao timu zao ziliibuka na ushindi katika michezo yao ya hatua ya makundi.
Mungaya alisema kuwa betPawa wanajisikia furaha kuwa wadau wakubwa wa kuendeleza mpira wa kikapu hapa nchini na kuwawezesha wachezaji, makocha na viongozi moja kwa moja kupitia Locker Room Bonus.
Alisema kuwa mashindano ya mwaka yamekuwa na ushindani mkubwa kutokana na uwepo wa Locker Room Bonus.
“Chapa yetu imewekeza Sh317 milioni kudhamini mashindano ya mwaka huu. Wachezaji mpaka sasa wamelipwa Sh91 milioni. Malipo haya yamefanyika moja kwa moja kupitia namba za simu za wachezaji mara tu mechi inapomalizika kupitia Locker Room Bonus (LRB) ambapo kila mmoja analipwa Sh140,000,” alisema Mungaya.
Alifafanua kuwa kupitia mpango huu wachezaji wameongeza morali, ushindani na kuleta uwajibikaji wa hali ya juu katika mashindano.
“Tunaimani ushindani utakuwepo zaidi katika hatua hii ya nusu fainali na fainali. Ni wazi kuwa kila mchezaji anataka kupata ‘mshiko’ wa ushindi kupitia LRB,” alisema Mungaya.
Kwa upande wake, Katibu mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Mwenze Kabinda aliipongeza betPawa kwa kuimarisha ustawi wa wachezaji na kuongeza hadhi ya mashindano ya NBL nchini.
Kabinda alisema kuwa ligi ya Taifa kwa sasa imekuwa na mvuto mkubwa na kuwavutia vijana wengi nchini kucheza mpira wa kikapu.